jump to navigation

Uchanga wetu ni kwa vigezo gani? December 8, 2006

Posted by Ramadhani Msangi in Siasa.
trackback

tanzania.gif

“ Ili tuendelee tunahitaji mambo manne; Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi bora….. Shaaamooo mwalimu”

Naam, hiyo ndio ilikuwa aina au staili yetu ya kusalimia wakati huo nipo darasa la sita katika Shule ya Msingi Usangi wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro. Kila darasa katika shule yetu lilikuwa na staili yake ya kusalimia kwa kukariri mistari iliyopatikana kutoka kwa marehemu (au hayati?) Azimio la Arusha.

Miaka mingi sana baadae ningali nikiikumbuka vyema mistari niliyokaririshwa katika madarasa yote niliyopitia katika shule hiyo. Na sio kuyakumbuka tu, bali kuyakumbuka yakiwa na nguvu kubwa mno ndani yangu bilashaka kuliko ilivyokuwa wakati huo nakaririshwa na akina Marehemu Mwl. Sudi, Mw. Diwani, Mwl. Rose na wengine wengi. (Popote mlipo walimu wangu nawakumbuka sana na ninawapenda sana)

Katika zama hizo za miaka mingi sana baadae, Disemba 09, 2006, Tanzania itakuwa ikiadhimisha miaka 45 toka ilipopata ilipojichukulia Uhuru wake uliokuwa mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza. Miaka 45 kwakweli si haba. Huo ni wastani wa muda wa kuishi kwa binadamu katika baadhi ya mataifa hapa duniani (hivi Tanzania tuko hapo?). Waliozaliwa mwaka ule wa uhuru wanaweza kutueleza hili kwa uzuri zaidi.

Wakati maadhimisho haya yakifanyika hata hivyo, moja kati ya matatizo ambayo nadiriki kusema kuwa yamekuwa yakikua kulingana na ukuaji wa taifa letu ni lile la uchumi duni kuanzia katika ngazi ya taifa hadi ngazi ya mwananchi mmoja mmoja.

Na ingawa ni hulka ya mwanadamu kuwa sio lazima tukubaliane katika kila jambo, bado hata wale ambao wanaweza kupingana na hilo watakubaliana nami kuwa kile wenyewe wanachokiona kama hali nzuri ya kiuchumi haiendani kabisa na utajiri wa rasilimali ambazo nchi hii imebarikiwa, nikimaanisha utajiri wa ardhi yenye rutuba, mabonde yanayowezesha shughuli za kilimo kwa mwaka mzima, madini ya kila aina, mbuga za wanyama na nyingine lukuki uzijuazo wewe.

Miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa katika siku ya leo ni pamoja na hotuba za viongozi katika ngazi mbalimbali wakiwemo hata wanaoalikwa kuja kuungana nasi katika kusherehekea siku hii, na miongoni mwa vipoengele ambavyo kwakweli sitarajii vikosekane katika hotuba za viongozi wetu watakaopata nafasi ya kuongea leo ni pamoja na kile kinachohusu hali ya uchumi wan chi yetu.

Hiki ni kipengele muhimu ambacho kwa bahati mbaya sana kila mwaka kimekuwa kikikaribia natamani kuzima redio au hata luninga yangu nisisikie wakati wakikizungumzia. Ndio!! Nimeshachoshwa na hadhithi na ngonjera za kila mwaka kuhusu hali ya uchumi wa taifa hili.

“Taifa letu bado ni changa sana hivyo hata uchumi wetu bado ni mchanga ambao unakua kwa kasi hata hivyo, hata mataifa yaliyoendelea hayakuanza na kuwa tajiri kwahiyo tuwe na subira na tuendelee kushikamana katika kuhakikisha uchumi wan chi yetu inakua”

Haya ni baadhi ya maneno ambayo yamekuwa yakizungumzwa sana na watawala wetu kwa miaka nenda miaka rudi sasa. Hivi uchumi gain huu ambao ndio unakua lakini bado ni mchanga hata baada ya miaka 45 sasa? Hivi viongozi wetu wanaweza kutueleza kuwa miaka hiyo 45 iliyopita walikuwa wapi na sasa wako wapi ili waone tofauti na kubaini kuwa tulitakiwa kuziona tofauti hizo pia katika kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi hii?

Azimio la Arusha, linatueleza kuwa tunahitajika kuwa na mtaji wa Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi bora. Na ikiwa tutataka kuwa wakweli ndani yetu tutakubaliana kuwa tuna utajiri mkubwa sana wa Rasilimali watu na Rasilimali ardhi na kwamba matatizo yetu mengi sana yametokana na kirusi kibasa sana kilichovamia Rasilimali Siasa safi na rasilimali Uongozi bora. Virusi vya unafiki, uongo, ulafi, upenda madaraka, wizi na kila aina ya uozo ambao umevamia katika rasilimali hizo.

Hivi asilimia kubwa ya viongozi tulio nao hivi sasa walikuwa wapi kipindi hicho? Naamini kuwa wengi wao walikuwa katika rika la ujana na walithubutu kumtingisha mkoloni kiasi cha kuweza kuliletea taifa lao uhuru uliopo sasa. Wakiwa vijana, wao waliweza, lakini hivi sasa wanaona vijana hawafai, huu sio unafiki ni nini? Hivi kinacho washinda wao kukiri tu kuwa zama zao zimepita na huu ni wakatui muafaka kuachia vijana wenzao walio na damu na mitizamo inayochemka kama walivyokuwa wao wakati wanapigania uhuru, ni nini hasa?

Miaka 45 bado wanakwambia kuwa nchi ni changa mno hivyo hata uchumi wetu kuwa mchanga sio jambo la ajabu. Hivi udogo wa nchi hii mnaupima kwa vigezo gani hasa? Umri wenu mlio nao au? Maana kama mnapimia kwa umri wenu ni wazi kabisa kuwa kweli nchi hii sio tu kuwa ni changa bali itaendelea kuwa changa hadi siku mnaiaga na kurejea mavumbini.

Hatukatai inawezekana kweli umri huo ukawa mdogo katika kuimarisha uchumi ikiwa tunajilinganisha na hayo mataifa mnayosema yameendelea. Lakini je, mnadhani waliokuwa watawala wa mataifa hayo katika miaka 45 yao ya kama wangekuwa watu wa longolongo na usanii kama wenu, mataifa hayo yangekuwa hapo yalipo sasa?

Wenzenu walitumia miaka hiyo kwa ajili ya kuweka sera za kitaifa za kujikwamua toka walipokuwa, wakaweka dira na kutengeneza njia kwa ajili ya wajao kuelekea haraka kwenye mapinduzi na mageuzi ya kimaendeleo ya kiuchumi. Sasa nyie mbona mnajenga njia kwa ajili yaw ala rushwa, mnajenga mazingira ya taifa la ombaomba hadi kufa, mnatengeneza taifa lenye matabaka ya watakatifu na watakavitu?

Wadadisi wa masuala ya kiuchumi nadhani watakubaliana nami kuwa kwa kadiri ambavyo miaka imekuwa ikisonga mbele, hali imezidi kuwa mbaya pengine toka kipindi tunapata uhuru. Hata thamani ya pesa yetu imekuwa ikiporomoka kila uchao. Matabaka ya walio na wasiokuwa na elimu yamezidi kukua kila siku kama ilivyo kwa matabaka ya walio na wasio nacho. Na haya ndio mmeyafanya katika miaka hiyo 45.

Hivi uchumi utajengwa kweli na taifa lililojaa wala rushwa na mafisadi? Taifa lijengwe na wauza unga kweli? Taifa lijengwe na mkulima ambaye mmegoma kumsaidia jembe la kisasa ili aboreshe ulimaji wake huku nyie mkipuyanga na kuzurura na mashangingi yenu ya bei mbaya?

Ngonjera za wala rushwa kujulikana majina yao tumezisikia toka zama na zama, ngonjera za wauza unga kujulikana hazijaanza awamu hii, ngonjera za maisha bora pia, lakini ni lipi hasa ambalo mnaweza kujivunia kuwa mmelifanya kwa ukamilifu na utimilifu bila kudai au kujichetea marupurupu ma pasenti zenu kadhaa?

Mmoja kati ya wasanii wanaowika vilivyo nchini Tanzania almaarufu kwa jina la Mr. Ebbo, katika moja ya tungo zake kuna kipande anasema kuwa maji yaliyotulia ndio huzamisha watu. Ni vyema wakati watanzania tukiadhimisha miaka hii 45 ya uhuru wetu tulikumbuke hili kwa maana hata Punda akichoka hupiga mateke.

Yapo mengi sana ambayo tunaweza kuzungumza lakini kubwa la msingi ni kuwa, Watanzania wamechoshwa na longolongo na usanii mnaowafanyia, mlileta uhuru mkiwa vijana na nyie hamna budi kuwapa vijana nafasi muwe washauri tu maana imeonyesha wazi kuwa wakati wenu ulishapita, wengi wenu hamuwezi kwenda na kasi ya dunia ya sasa.

Mungu Ibariki Tanzania
Mungu Ibariki Afrika

Comments»

1. james - December 11, 2006

Mh!! Kweli kabisa yaani ni usanii ule ule wa zamani kwa ari, kasi na nguvu mpya. Wameanza kukimbia vivuli vyao sasa, wanasingizia mgao wa umeme waliukuta toka awamu iliyopita. Jamani hivi kweli enzi za Mkapa hali ilifikia kiwango hiki? Tanzania yenye neema nadhani itawezekana kwa mara ya kwanza hapa Tanzania ndani ya vibatali na taa za kandili kwa wenye nazo.

Hivi kaka Msangi hata magogoni nako kuna tatizo la mgao wa umeme au yale makelele ya jenereta kama huku uswalihili?


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Follow

Get every new post delivered to your Inbox.